Kazi Zetu‎ > ‎

Njia Zetu za Kazi

Iwapo utapenda kusoma zaidi kuhusu njia zinazotumika na Daraja katika kazi zake tafadhali fungua hapa usome Maelezo mafupi kuhusu mawazo yetu ya awali (concept Paper, 2007).
 
Daraja ni shirika jipya lisilo la kiserikali, lenye nia  ya kufanya taasisi zilizoko wilayani na vijijini ziwajibike zaidi kulingana na mahitaji ya jamii. Lengo letu ni kuziwezesha jamii na taasisi mbalimbali kufanya kazi kwa ushirikiano ipasavyo na hatimaye kuchangia katika kupunguza umaskini vijijini Tanzania.
 
Tunaamini kuileta serikali karibu zaidi na wananchi, na kuwa na serikali ye kidemokrasia inatoa nafasi kubwa kwa jamii yoyote ile kuwa na uhuru na haki sawa. Kutokana na sababu hizi za msingi Daraja inajituma katika kuhakikisha mfumo wa demokrasia katika ngazi ya wilaya na kijiji unafanya kazi kiufasaha kwa kusaidia jamii zilizo maskini nchini Tanzania.
 
Sisi Daraja tutafanya kazi zifuatazo:
  • Kufanya kazi na serikali za mitaa
    , ili watumishi waweze kuzingatia zaidi maslahi na matakwa ya jamii
  • Kufanya kazi na wanajamii, ili watambue zaidi haki zao na kuweza kuihimiza serikali iwajibike zaidi kwao
  • Kuboresha mawasiliano kati ya serikali na jamii, kwa mfano kuandaa nafasi za mijadala na majadiliano
Matatizo na Yapi?
 
Upungufu wa fedha siyo tatizo kubwa linalozuia maendeleo katika maeneo ya vijijini Tanzania kwa sasa. Mapato ya ushuru yameongezeka sana kutokana na kukua kwa uchumi, na wafadhili wanaendelea kumwaga pesa hapa nchini na kiwango ambacho kinacho ongezeka siku hadi siku. Ingawa asilimia kubwa ya pesa hizi hazijaelekezwa vijijini, bado kuna fedha za kutosha kuboresha huduma za jamii pamoja na kupunguza umaskini.
 
Hivyo, kwa nini hatuoni mabadiliko ambayo kila mmoja anatarajia? Tafiti zetu zimeonyesha matatizo machache yanayozuia serikali za wilaya na mitaa zisiweze kuwajibika ipasavyo. Matatizo haya ni pamoja na:
  • Wananchi hawana njia rahisi kufanya serikali iwajibike kwao. Mfumo wa vyama vingi ni hatua ya kwanza tu. Kuna uhaba wa wagombea wenye mawazo tofauti na uhaba wa majadiliano wazi katika jamii juu ya vipaumbele vyao. Vyombo vya habari ni vichache na asasi zisizo za kiserikali hazina nguvu.
  • Serikali ya Taifa, pamoja na wafadhili, hawajaziachia Halmashauri za Wilaya mamlaka ya kufanya uamuzi wenyewe. Kwa njia tofauti tofauti, halmashauri zinajikuta zimebanwa. Hii inatokea kwa sababu ya hofu za watu wa juu ya uwezo na rushwa, nk, lakini matokeo yake ni kuwa halmashauri hawazingatii maslahi ya jamii: nani angepoteza muda wake kupeleka mapendekezo yake wilayani kama anajua maamuzi juu ya maswala makubwa yote yanatokea taifani?
  • Utamaduni wa utawala katika ngazi ya wilaya huwa unazuia utawala bora. Katika historia, kazi ya serikali ya wilaya na mitaa ilikuwa kutekeleza mipango inayotokea katika wizara za taifa badala ya kusikiliza mawazo ya wananchi. Pia, wananchi hawajazoea kutoa hoja au kuchambua kazi za serikali.

Daraja Itafanya Nini Kupambana na Haya?
  
Katika ngazi ya kijiji na wilaya - tutaongeza nafasi za majadiliano juu ya mahitaji na matakwa ya jamii, ili kusaidia jamii kutambua vipaumbele. Tutaelimisha jamii juu ya haki zao, hasa kwa vikundi vinavyokumbwa na matatizo zaidi. Pia, tutashirikiana na serikali kuwaongezea uwezo wa kushirikisha jamii.  
 
Katika ngazi ya taifa - tutafanya utafiti juu ya matokeo ya miradi kama yetu na kusambaza ujuzi na uelewa unaotokana na utafiti huu. Pia tutafanya utafiti juu ya utekelezaji wa sera za kitaifa katika ngazi za wilaya na kijiji, na kutumia utafiti huu kushauri serikali juu ya namna kuboresha sera ili kuhakikisha halmashauri zizingatie zaidi maslahi na matakwa ya jamii.